Your are here: Home // Habari // UBINAFSI NDIO KIFO CHA TASNIA YA FILAMU TANZANIA – MKINDI

UBINAFSI NDIO KIFO CHA TASNIA YA FILAMU TANZANIA – MKINDI

Bongo Movie

Wasanii wa Filamu Swahilihood wakiandamana

Na Ignas Mkindi
HARAKATI za kupigania tasnia ya filamu Tanzania zinazidi kuchukua sura mpya kila uchwao kutokana na siri iliyopo nyuma ya wale ambao wanakuwa mbele ya harakati hizi ambao inaonekana mara zote wanahitaji makundi ili kufanikisha maslahi yao, kila mtu amekuwa Adui wa Yule anayeonekana kuwa na mawazo chanya dhidi ya harakati hizi.

machinga Kariakoo

Machinga wakilalamika kuzuiwa kuuza filamu za nje

Bongo Movie

Wasanii wa Bongo Movie wakiandamana.

Maduka Kariakoo

Askari wakilinda maduka yaliyofungwa baada ya kukamatwa

Nape Nnauye.

Mh. Nape aliyekuwa Waziri wa Habari na Utamaduni Sanaa Michezo akiendesha Oparesheni Kariakoo.

“Ili tuwe wamoja inabidi tuwe na lengo moja na mtazamo unaofanana katika kufikia lengo hilo na hayo yanawezekana tu endapo tutaelimishana kwanza,”anasema Mkindi.

Tumekuwa tukilalamika kutokana na matatizo ambayo yanatukabili na kutuzuia kufanikiwa katika tasnia hii tuliyojiajiri, matatizo kama filamu za nje zisizofuata utaratibu, wizi wa kazi zetu, wasambazaji kulazimisha kununua hakimiliki, kukosa ruhusa ya kutumia baadhi ya mandhari za kupigia picha, kutoruhusiwa kutumia mavazi yanayofanana na majeshi yetu, mrundikano wa kodi na tozo mbalimbali na matatizo mengine mengi lakini kubwa zaidi tukiilalamikia serikali kuwa haitusapoti katika kuinua tasnia yetu.

Inatubidi tuelewe kwamba serikali ipo kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu, inapanga vipaumbele vyake kwa kuzingatia sera mbalimbali na inafanya kazi zake kwa kufuata sheria.

Sasa kwa filamu, kundi letu halitambuliwi katika katiba ya sasa, hakuna na hakujawahi kuwa na sera ya filamu na kubwa zaidi sheria yake ya mwaka 1976 imepitwa na wakati.

Mpaka hapo utaona fika kuwa hakuna lolote tunaloweza kulipata toka serikalini na yote tunayoahidiwa na wanasiasa ni propaganda tu ili tuweze kuwasapoti kwenye chaguzi mbalimbali, na bahati mbaya wanasiasa wanatuona sisi ni mamburura na tunawadhihirishia umburura wetu kwa kukubali ahadi zao za kusubiri meli uwanja wa ndege.

Serikali inayotaka kutengeneza Tanzania ya viwanda inawezaje kuacha kiwanda kikubwa zaidi kuliko vyote kinachotoa mamilioni ya ajira kikielekea kufa kwa tatizo ambalo mchakato wa utatuzi wake hauwezi kuchukua hata miezi mitatu kukamilika endapo serikali itakuwa na dhamira ya kweli kukiokoa?

Watayarishaji wa filamu tulio na fursa ya kuonyesha kazi zetu katika vituo mbalimbali vya televisheni za kimataifa huku pia nakala za DVD za kazi zetu zikifika nchi mbalimbali kwa njia halali na haramu hatuna sehemu za kupatia mitaji ya kutengeneza kazi nzuri na za uhakika wakati huo huo kuna mamlaka zinazosimamia utalii, vivutio vya nchi,

utamaduni wetu na mambo mengi zinatumia mamilioni ya kodi ambazo na sisi tunachangia kulipia matangazo badala ya sehemu ya fedha hizo kutengwa ili tutengeneze kazi bora katika maeneo ya vivutio vya nchi kwa ajili ya kuvitangaza.

Kuna maktaba zinazokodisha kazi za filamu, kuna maduka yanayouza kazi za filamu, kuna mabanda yanayoonyesha kazi za filamu na yote hayo yako katika mitaa yetu ambayo kuna ofisi za serikali za mitaa lakini serikali inashindwa kuyatambua na kuyaoroshesha wakawa wateja wetu wa uhakika wakati huo huo kuna mamilioni ya kodi zetu

yanayotumika kwa elimu kwa umma kuhusiana na masuala mbalimbali ambayo sehemu kidogo tu ya fedha hizo zingetumika kujenga mfumo na kutumia filamu zetu kupeleka elimu inayokusudiwa au kwa kuweka matangazo au kuwa sehemu ya filamu husika.

Haya na mengineyo yanayoweza kuinua tasnia ya filamu hayawezi kutekelezeka bila Sera ya filamu, madadiliko ya sheria ya filamu ya 1976 iliyopitwa na wakati na kuwekwa kanuni zinazoendana na mazingira halizi ya tasnia ya filamu kwa sasa.

Serikali inayoingiza mapato kutokana na tozo za vibali vya kupiga picha, ukaguzi wa filamu, usajili wa kazi, Clearance, malipo ya stempu za TRA, kodi ya mapato kutokana na nakala zinazouzwa na kodi nyingine mbalimbali kwa mujibu wa sheria zinazolipwa na makampuni yanayojihusisha na uuzaji wa vifaa vya kutengenezea filamu,
utengenezaji na usambazaji wa filamu inashindwa kupitisha tu Sera ya filamu ambayo wadau wenyewe kupitia Shirikisho la Filamu Tanzania
(TAFF)

kwa kuona umuhimu wake walifanya utafiti na kuandika rasimu kwa kutumia zaidi ya milioni mia mbili na kuikabidhi serikalini tangu mwaka 2013 na inashindwa kupitisha marekebisho ya sheria ambayo tayari wadau tulishaitwa kutoa maoni kwa siku tatu uwanja wa taifa toka mwaka 2009 kwa gharama za serikali.

Masuala ya kutatua changamoto za tasnia ya filamu yamekuwa kama homa za vipindi kutokana na waziri aliyepo. Alipokuwepo Komredi George Mkuchika tulianza kupata mwanga na sheria ikaanza mchakato wa kubadilishwa ikafikia hadi hatua ya kutaka kupelekwa kupitishwa kwenye kikao cha makatibu wa wizara, alipoondoka ikatupwa kabatini ukimya ukarudi kama zamani. Kuingia mh. Nape kaanza kusukuma vyote kwa hatua kuanzia na sera, sasa kaingia mhe. Mwakyembe kajikita kwenye ‘marufuku’ tu.

Ndugu zangu wadau wa filamu, kwanini tunaedelea kuukenulia meno unafiki wa wanasiasa kama mataahira? Nadhani siku tutakapoingia location bila kibali ambacho kinapatikana bodi ya filamu kwa laki tano halafu tukakamatwa kuanzia mtayarishaji, mwongozaji na wengine wote tukafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la jinai la kutengeneza filamu bila kibali cha waziri kama sheria ya 1976
inavyotaka ndipo tutakapojua ubaya wa nyoka tunayemfuga.

filed under: Habari

Leave a reply

Home | About us | Contact us| Privacy Policy | Terms of use | Copyright © 2010 swahili hood portal . All rights reserved.
  • Facebook